MGOMBEA
Urais wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) ambaye pia anaungwa mkono
na vyama vya NCCR-Mageuzi, CUF na NLD, Edward Lowassa amesema endapo
atachaguliwa kuwa rais ataunda serikali isiyokuwa ‘nyoronyoro’.
Akiwahutubia
wananchi wa Jimbo la Kawe jijini Dar es Salaam katika viwanja vya Shule ya
Msingi Bunju ‘A’, Lowassa alisema muda umefika kwa wananchi wa Tanzania kufanya
mabadiliko.
“Naombeni
mniteue niwe rais wenu ili mpate maendeleo ambayo hamkuwahi kuyapata kwa
kipindi cha miaka zaidi ya hamsini. “Mimi nitaunda serikali isiyokuwa
nyoronyoro na inayofanya kazi zake kwa ufanisi na kila mtanzania ataweza
kunufaika na rasilimali za nchi yake,” alisema Lowassa aliyehutubia kwa
takribani dakika kumi.
Alisema
endapo atafanikiwa kuwa Rais wa Awamu ya Tano, serikali yake itafanya kazi kwa
spidi ya mwendo kasi wa 120 na hivyo lazima kutakuwa na maendeleo makubwa kwa
muda mfupi.
“Nitaondoa
changamoto zote zinazowakabili wananchi wa Tanzania, ikiwemo ukosefu wa huduma
ya maji safi na salama katika maeneo mengi hapa nchini, nitatatua changamoto ya
mazingira ya kufanyia biashara ndogondogo pamoja na kutoa elimu bure,” alisema
Lowassa.
Aidha,
aliwahakikishia wananchi kuwa wasiwe na hofu kuwa kura zao zitaibwa, akisema,
“Hakuna atakayeiba kura ng’o. Nimesikia kuwa kuna njama za kuiba kura, hakuna
jambo kama hilo, bali kila mtu akipiga kura ahakikishe analinda kura hadi
mwisho ili kutoruhusu mwanya wa kuiba na hakuna atakayeiba kura ng’o.”
Awali,
akimkaribisha Lowassa, Mwenyekiti wa Chadema Taifa, Freeman Mbowe alisema wamezunguka
katika baadhi ya maeneo ya nchi na kuona watanzania wamechoka na ugumu wa
maisha na hivi sasa wanataka mabadiliko.
“Watanzania
wanahitaji mabadiliko, tumepata mapokezi makubwa sana kila tulipopita kuomba
ridhaa ya wananchi, hii inaonesha ni jinsi gani wananchi hawa wapo tayari
kukombolewa,” alisema Mbowe.
Mbowe
aliwataka wananchi wajitokeze kwa wingi kwenda kupiga kura na kuchagua Chadema
ili kiwakomboe na kutatua changamoto zinazolikabili taifa. Baada ya kutoka Kawe
katika Manispaa ya Kinondoni, jioni Lowassa alikwenda katika jimbo lingine la
manispaa hiyo, Kibamba, kuendelea na mkutano wa kampeni.
Imeandikwa
na Emmanuel Ghula
0 comments:
Post a Comment