MGOMBEA
urais kupitia Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), chini ya
mwamvuli wa Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa), Edward Lowassa,
ameisimamisha tena Dar es Salaam kwa saa kadhaa huku akiwataka
Watanzania kutokosa usingizi kwani hakuna kura itakayoibwa.
Lowassa
alisema hayo jana jijini Dar es Salaam kwa nyakati tofauti alipokuwa
kwenye mikutano ya kampeni Wilaya ya Kinondoni katika majimbo ya Kawe na
Kibamba.
Akiwa
katika mkutano uliofanyika katika viwanja vya Shule ya Msingi, Bunju A
kwenye Jimbo la Kawe, alisema watu wasikose usingizi bali wasubiri
Oktoba 25 ifike.
Licha ya
kwamba Lowassa alifika Bunju saa saa 9:25 alasiri, viwanja hivyo
vilianza kufurika watu kuanzia asubuhi kwani mkutano ulitarajiwa kuanza
saa 5:00 asubuhi.
Hali
ilikuwa hivyohivyo kwenye Jimbo la Kibamba ambako licha ya kiongozi huyo
kufika katika eneo hilo saa 11:30 jioni, watu walianza kufurika
asubuhi, hali iliyofanya barabara ya Morogoro kupitika kwa shida.
MSIKOSE USINGIZI
Akizungumza
katika Mkutano wa Kawe, Lowassa alisema shaka dhidi ya Tume ya Taifa ya
Uchaguzi (NEC), iliyopo sasa inatokana na jeuri ya wapinzani wao.
“Kuna
maneno mengi yanasemwa kuhusu NEC... nawahakikishieni hawataiba ng’o,
tuko imara, tutalinda kura zetu hadi zitakapohesabiwa.
“NEC na CCM hamtaweza kuiba kura zetu, Watanzania tukatae kuibiwa kura na kulaghaiwa,” alisema Lowassa.
Aidha
Lowassa alisema kuna watu wa ofisini wanataka mageuzi, lakini
wanatishwa, na wengine ni wafanyabiashara wanaotaka kutusaidia.
“Hao wanaowatisha walie tu, hawawezi kumshughulikia mtu yeyote,” alisema.
Alisema atabadilisha mfumo wa utendaji kazi wa Serikali kutoka ulivyo sasa na kuwa wa kasi. “Itakuwa ni spidi 120”, alisema.
Aliendelea
kusema: “Zimebaki siku 48, tukatae msongamano wa magari Dar es Salaam,
adha na tabu katika hospitali na vituo vyetu vya afya, michango ya shule
za sekondari na msingi, tatizo la maji na ajira.
“Fanyeni
uamuzi mgumu tuibadilishe wizara ya elimu, tuwe na kilimo cha kisasa na
kuanzisha viwanda kwa ajili ya vijana wetu nchini,” alisema.
SUMAYE
Waziri
Mkuu Mstaafu, Frederick Sumaye alipanda jukwaani saa 9:55 alasiri na
kuonya kuwa kama CCM haitakubali kushindwa inaweza kusababisha
machafuko.
“Nchi hii
iko kwenye mfumo wa vyama vingi na ili viwe na maana lazima kila chama
kiwe tayari kushindwa kama hakijafanya vizuri, lakini CCM hakitaki, hali
hii ni hatari sana.
“Libya,
Misri na Tunisia zimefika zilipofikia kwa sababu waliokuwa kwenye
madaraka walikuwa hawataki kuachia na kukandamiza watu. CCM isipokubali
mabadiliko itakuwa inataka yale ya Gadafi,” alisema Sumaye.
Alifananisha matusi yanayotolewa na wapinzani wao dhidi yake na Lowassa kuwa ni sawa na kumpiga teke chura.
“Wanatengeneza
timu za kututukana, lakini nawaambia hapo ni sawa na kumpiga teke
chura. Lowassa alitoka serikalini miaka minane iliyopita na tume ya
Bunge ilisema hakukuwa na jambo lililomgusa moja kwa moja...alijitosa
ili kumuokoa rais na Serikali yake,” alisema.
Waziri
Mkuu huyo pia aliibeza hoja ya mgombea urais wa CCM, Dk. John Magufuli
kuwa hataweza kupambana na rushwa kwa sababu tayari ameonyesha udhahifu
katika wadhifa aliokuwa nao wa Waziri wa Ujenzi.
“Utabadilishaje Tanzania wakati leo hii wewe ni waziri, lakini kwenye mizani kumejaa rushwa?
“Ataitoa wapi nguvu ya kupambana na rushwa, ndani ya CCM huwezi kufanya kitu chochote,” alisema.
Sumaye
pia alisema kitendo cha kutoweka jina la chama katika mabango ya mgombea
urais wa CCM kinaonyesha kuwa ndani ya chama hicho hali ni mbaya.
“Mabango yanasema “Chagua Magufuli” hayasemi “Chagua CCM”, kama anajua CCM haimpeleki kokote si angekuja Ukawa?
“Mimi niko Ukawa, lakini sigombei urais, kazi yangu ni kuwakomboa wananchi,” alisema Sumaye na kuongeza kuwa “CCM ni shida”.
MBOWE
Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe, alitamba kuwa wananchi wote wako tayari kufanya mabadiliko.
“Tumekwenda
Iringa, Njombe, Ruvuma, Rukwa, Katavi, Kigoma, Tabora na leo (jana)
tuko Dar es Salaam, nchi imeshalegea na iko tayari kwa sababu ya
Lowassa,” alisema Mbowe.
Huku
akiwaelekeza wananchi kuzungusha mikono kama ishara ya kufanya
mabadiliko, Mbowe alionya kuwa kama machafuko, basi yataletwa na NEC
kutokana na kitendo chao cha kujaribu kuibeba CCM.
“Sasa
hivi CCM haibebeki hata ukileta mbeleko, wanawatumia baadhi ya watu
kumchafua Lowassa, Sumaye na wote walioondoka CCM...wapuuzeni watu
wamefika bei,” alisema.
MDEE
Mgombea
ubunge katika Jimbo la Kawe, Halima Mdee, aliomba idhini ya viongozi wa
chama hicho kufanya maandamano ya kuishinikiza NEC kuacha kufanya
hujuma.
“Tuna
mashaka na zoezi linaloendelea la uhakiki, kuna watu wanaandikisha
vitambulisho vya vijana na kina mama, CCM na NEC wanataka kufanya uhuni.
“Tunaomba kauli yenu kama ikibidi tuandamane hadi NEC tukakinukishe, tutafanya hivyo,” alisema Mdee.
Kwa
mujibu wa Mdee,katika jimbo hilo wamefanikiwa kutatua migogoro ya ardhi
katika eneo la Chasimba na Nakerekwa, lakini bado kuna mgogoro katika
eneo la Boko kwa Sonji ambao umedumu kwa zaidi ya miaka 20 na katika
eneo la Magereji lenye vijana zaidi ya 4,000.
“Mtaji wa
vijana hawa wa gereji ni zaidi ya Sh bilioni tano na wamekaa hapa tangu
mwaka 2007, lakini leo hii wanaambiwa waondoke,” alisema.
MWALIMU
Naibu Katibu Mkuu wa Chadema-Zanzibar, Salum Mwalimu, alisema CCM wameishiwa sera na sasa wanafanya matamasha ya burudani.
“Magufuli
anazunguka nchi nzima kufanya matamasha ya burudani badala ya kunadi
ilani ya chama chake...ukiingia muachie wizara ya utamaduni,” alisema
Mwalimu.
KUWASILI UWANJANI
Maelfu ya wananchi walianza kuwasili viwanjani hapo saa 3 asubuhi na ilipofika saa 7 mchana uwanja ulikuwa umejaa.
Baadhi ya
watu walilazimika kupanda juu ya miti na wengine kupanda juu ya mapaa
ya Shule ya Msingi Bunju A ili waweze kushuhudia matukio mbalimbali
yaliyokuwa yakiendelea katika mkutano huo.
Waendesha
bodaboda walikuwa ni kivutio pekee katika mkutano huo kwani wengine
walionekana kuendesha pikipiki kwa mbwembwe kubwa huku wakipaa juu na
wengine walikuwa wakizunguka uwanja huo mara kwa mara.
Baadhi ya
watu walikuwa wamebeba mabango yenye ujumbe mbalimbali kama vile ‘Dk.
Slaa kiapo cha kanisa kimekuponza uchizi unakunyemelea’ na ‘ulipo tupo’.
JIMBO LA KIBAMBA
Katika
mkutano uliofanyika Jimbo la Kibamba kwenye Uwanja wa Mbezi Mwisho,
Lowassa alisema hana muda wa kubishana na wanachama wa CCM wanaomtukana
majukwaani, na kwamba watakutana katika sanduku la kura.
“Mahaba
yananifanya nijiamini, ndiyo maana ndugu zangu wanahangaika nikiwa na
nguvu ya umma kama hii, nawaambia tukutane kwenye sanduku la kura,”
alisema.
Lowassa
alisema endapo watu wanataka mabadiliko katika maeneo mbalimbali ikiwamo
elimu, wanapaswa kuandaa shahada zao na kuwapigia kura wagombea wa
Ukawa Oktoba 25.
Naye Sumaye alisema katika uchaguzi wa mwaka huu CCM lazima itoke madarakani hata kama haitaki.
“CCM
hakitaki kutoka madarakani hata kama watu hawakitaki, wanatumia hila
zote, tunasema safari hii mtatoka tu ,mnahangaika kuchafua viongozi,
mnanihangaika hadi mimi ambaye sigombei,” alisema Sumaye.
Alisema kitendo cha wanachama wa CCM kujipanga na kumtukana hakisaidii badala yake kinamwongezea nguvu ya kupigania maendeleo.
Sumaye alisema alikihama chama hicho kwakuwa kimeshapoteza matumaini ya kuleta maendeleo kwa wananchi.
MNYIKA
Mgombea
ubunge Jimbo la Kibamba, John Mnyika, alimfanisha aliyekuwa Katibu Mkuu
wa Chadema, Dk. Willibrod Slaa na Samson wa kwenye Biblia aliyedanganywa
na Delila.
“Mnamfahamu
Samsoni wetu? Alisema tumemchukua mtu chooni tukamwingiza chumbani,
amesahau kwamba yeye katoka chumbani ameenda chooni, msiendelee
kumsikiliza Samsoni, mpuuzeni hana jipya.
“Mzee wetu kadanganywa ameenda chooni kuwaunga mkono CCM,” alisema Mnyika.
Katika
hatua nyingine, alimtaka Lowassa akiingia madarakani kuangalia tatizo la
maji ambalo ndilo kubwa ndani ya jimbo la Kibamba.
Naye
Mwenyekiti wa Chadema, Mbowe, aliituhumu CCM kuwa inatumia Mamlaka ya
Kodi Tanzania (TRA) kukwepa kodi ya mafuta ili ikusanye Sh bilioni 50 za
kununua shahada za kupigia kura.
“Kuna
mkakati wa kuitumia TRA kuingiza mafuta ambayo hayatalipiwa kodi ili
wapate Sh bilioni 50 kwa ajili ya kuwasaidia kununua shahada za kupiga
kura. Tunawaambia tumewabaini na waache mara moja huo mchezo, tunataka
watukabidhi nchi ikiwa na hazina ili tuweze kuleta mabadiliko ya kweli,”
alisema Mbowe.
Alisema anao ushahidi ju ya hilo na kuongeza kuwa CCM inaweweseka mwaka huu.