MWENYEKITI
wa Taifa wa Jumuiya ya Wazazi ya CCM, Abdallah Bulembo, ameonya juu ya siasa za
udini na ukabila kwenye kampeni na kuitaka Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC),
kuchukua hatua dhidi ya mgombea urais wa Chadema, Edward Lowassa.
Alisema
hayo jana kwa nyakati tofauti kwenye mikutano ya kampeni ya mgombea urais wa
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM), Dk John
Magufuli.
Alisema
hayo katika wilaya za Mvomero mkoa wa Morogoro na Kilindi mkoani Tanga. Bulembo
ambaye ni sehemu ya timu ya kampeni ya mgombea huyo wa Urais alisema: “Hili
haliwezi kuvumiliwa. Wahusika wachukuliwe hatua.” Pia, alishauri waangalizi wa
kimataifa wa uchaguzi mkuu wa Tanzania, utakaofanyika Oktoba 25 mwaka huu
kuliweka katika kumbukumbu zao suala kuingiza udini katika kampeni.
Kwa
upande wake, akihutubia katika maeneo mbalimbali ya wilaya hizo za Mvomero na
Kilindi, Dk Magufuli aliwataka Watanzania kuwakataa wanasiasa, wanaojaribu
kusaka madarakani kwa misingi ya dini na ukabila.
Alisema
kwa asili, Watanzania ni wamoja, hivyo hawapaswi kukubali kurubuniwa na
wanasiasa wanaojaribu kutumia kila njia kuhakikisha wanatimiza kiu ya kupata
`ukubwa’.
“Watanzania
ni wamoja, kamwe wasiwakubali kurubuniwa na pia wasimkumbatie yeyote anayefanya
siasa zenye lengo la kuwagawa iwe kwa udini au ukabila…hawa watatufikisha
pabaya,” alisisitiza Dk Magufuli.
Kauli
hizo za Bulembo na Magufuli ambaye pia ni Waziri wa Ujenzi, zimekuja baada ya
kuwapo kwa taarifa kuwa mgombea urais wa Chadema, Edward Lowassa juzi Jumapili
kujipigia debe kanisani kwamba yeye anastahili kuwa Rais wa Tanzania kwa sababu
ni Mkristo wa madhehebu ya Kilutheri, ambalo halijawahi kutoa Rais tangu taifa
hili lilipoundwa.
Lowassa
kanisani
Lowassa
alidaiwa kuyasema hayo akiwa katika Kanisa la Kiinjilili la Kilutheri (KKKT )
la Tabora mjini juzi Jumapili.
“Naomba
mniombee, mniombee kwelikweli. Nyie Walutheri mna sababu ya kuomba zaidi. Kwa
sababu tangu nchi hii iumbwe haijapata kutoa Rais Mlutheri. Mwalimu Nyerere
alikuwa Mkatoliki, Rais (Benjamin) Mkapa alikuwa Mkatoliki. “Sasa nadhani Mungu
atatuongoza ili nasi tuweze kuipata nafasi hiyo. Kwa hiyo naomba mniombee sana”
alisema.
Kwa
mujibu wa picha za video, zilizosambazwa katika mitandao mbalimbali ya kijamii
pamoja na watumiaji wa simu za mkononi zenye mtandao wa WhatsAPP, Lowassa
alitumia sekunde 23 kueleza maneno yake hayo na baadaye alisikika akianza
kuimba nyimbo.
Picha
hiyo ya video inaonekana kupigwa na mmoja wa waumini, waliokuwepo kanisani
wakati Lowassa akizungumza. Video hiyo iliyosambazwa na mtu asiyejulikana,
inamwonyesha Lowassa akiwa amevalia shati lake la rangi ya bluu na akizungumza
kwa kutabasamu mbele ya waumini wa kanisa hilo.
Hotuba
hiyo fupi ya Lowassa iliyomalizwa kwa pambio, haikutaja pia kwamba zaidi ya
Nyerere na Mkapa, Tanzania pia imewahi kuwa na marais wengine wasio Wakristo;
Ali Hassan Mwinyi na Jakaya Kikwete.
Mshindani
mkuu wa Lowassa katika Uchaguzi Mkuu wa mwaka huu, Dk John Magufuli wa Chama
Cha Mapinduzi (CCM) si Mlutheri kama Lowassa, hivyo mgombea huyo wa vyama vinne
vinavyounda Ukawa, alikuwa akitumia dhehebu lake kujipatia faida dhidi ya
mpinzani wake huyo. Mbali na Chadema, vyama vingine vinavyounda Ukawa ni CUF,
NCCR-Mageuzi na NLD.
Makamba
anena
Katibu
Mkuu za zamani wa CCM, Yusuf Makamba, alisema mara nyingi wanasiasa wanaoishiwa
mbinu, hukimbilia kuwagawa watu kwa misingi ya udini.
Kwa
mujibu wa sheria za uchaguzi hapa nchini, wagombea wa nafasi zote za kisiasa
hawaruhusiwi kufanya kampeni katika nyumba za ibada au kufanya siasa,
zinazochochea ubaguzi wa aina yoyote.
Taarifa
ya Tume ya Uchaguzi
Wakati
huohuo, Mwenyekiti Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC), Jaji mstaafu Damian Lubuva
amevitaka vyama vyote vinavyoshiriki katika uchaguzi mkuu, kuzingatia maadili,
huku akisisitiza Tume isilazimishwe kuchukua hatua za kutoa adhabu kwa vyama na
wagombea.
Badala
yake, amesisitiza kuwa busara itumike katika mikutano yote ya kampeni,
zinazotarajiwa kufikia ukingoni Oktoba 24 mwaka huu, baada ya kuwa
zimezinduliwa rasmi Agosti 22.
Katika
taarifa yake kwa vyombo vya habari, jijini Dar es Salaam jana, Jaji Lubuva
alisema licha ya kuwa kampeni zimeanza katika sehemu nyingi nchini, Tume
imeanza kupokea malalamiko kadhaa, hivyo kuvitaka vyama na wagombea kuwa makini
katika kuzingatia Sheria, Katiba na Maadili ya Uchaguzi wa Rais, Wabunge na
Madiwani ya mwaka 2015.
Alisema;
“Tangu Kampeni zianze, nafurahi kusema kwa niaba ya Tume kuwa kwa ujumla,
Kampeni zimeenda vizuri. Karibu mikutano yote imefanyika katika hali ya utulivu
na amani. Hatujapata taarifa ya mkutano wa kampeni ambao umevurugwa kwa fujo
zozote. Kwa hilo napongeza vyama vyote vya siasa. “Hata hivyo, kutokana na mikutano
hiyo nchini ya kampeni ngazi ya urais, ubunge na udiwani yamejitokeza mambo
ambayo ni kinyume kabisa na Mwongozo wa Maadili ya Uchaguzi wa Rais, Wabunge na
Madiwani wa mwaka 2015 uliotiwa saini na Vyama vyote vya Siasa tarehe 27 Julai,
2015.”
Alieleza
kuwa baadhi ya mambo yaliyojitokeza katika kampeni hizo ni kutozingatia muda wa
kumaliza mikutano ya kampeni, kubandika mabango ya kampeni, matangazo au mchoro
wowote kwenye maeneo yasiyoruhusiwa au bila idhini ya wahusika, kuchafua,
kubandua au kuharibu matangazo au picha za kampeni za vyama vingine na pia
kuwapo kwa matumizi ya lugha zisizo za staha.
Kutokana
na kuibuka kwa mambo hayo, alisema viongozi wa vyama vya siasa na wagombea wana
wajibu wa kisheria wa kuyaheshimu, kuyasimamia na kuyatekeleza maadili ya
mchakato wa uchaguzi, huku wakiwajibika pia kuwaelimisha, kuwahamasisha na
kuwasisitiza wanachama wao kutekeleza Sheria ya Uchaguzi.
Kinyume
cha hapo, alisema adhabu za ukiukwaji wa maadili ya uchaguzi, zinaweza kutolewa
hivyo kuweza kusababisha chama au mgombea kuathirika kwa namna moja ama
nyingine, ikiwa ni pamoja na chama au mgombea kusimamishwa kuendelea kufanya
kampeni.
Adhabu
nyingine imeelezwa kuwa chama au mgombea anaweza kuzuiliwa kutumia vyombo vya
habari, na wakati mwingine chama au mgombea anaweza kulipishwa faini ya hadi Sh
milioni moja.
“Katika
kipindi hiki cha kampeni, Chama au Mgombea akipewa mojawapo ya adhabu hiyo,
kunaweza kuathiri kampeni zake za kuelekea uchaguzi wa Rais, Wabunge au
Madiwani,” alisema Jaji Lubuva.
0 comments:
Post a Comment