MGOMBEA urais wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Dk. John Magufuli, amewataka wagombea ubunge na udiwani kupitia chama hicho, kutowabagua watu watakaowachagua kwa itikadi za vyama vyao.
Alisema suala la maendeleo halibagui, hivyo wana wajibu wa kumsikiliza kila mtu badala ya kusukumwa na itikadi za vyama.
Akizungumza katika mikutano yake ya kampeni mkoani Ruvuma jana, Dk. Magufuli alisema uongozi unahitaji uvumilivu na kwamba yeye atakuwa rais wa Watanzania wote.
Alisema katika kuhakikisha anaendesha nchi, amejipanga kuwaunganisha Watanzania ili waweze kuonja furaha ya maendeleo.
“Mimi nitakuwa rais wa Watanzania wote bila kujali itikadi zao, sitawaongoza kwa kiburi na majivuno, ila ninasukumwa na maendeleo ya kweli.
“Nanyi wana CCM ninawaambia, mnapoomba uongozi na mkichaguliwa, hamtakiwi kuwabagua wananchi kwa itikadi zao za vyama.
“Ndiyo maana mimi nimejipanga kuongoza Tanzania mpya, ambapo nitakuwa rais wa Chadema, CUF, NCCR-Mageuzi na hata wana CCM pamoja na wale wasiokuwa na vyama,” alisema Dk. Magufuli.
Alisema yeye si mwanasiasa ila mtendaji aliyejiandaa kuliongoza Taifa kisayansi.
KAPTENI KOMBA KUENZIWA
Akiwa wilayani Nyasa, Dk. Magufuli, alisema atahakikisha Serikali yake inamuenzi aliyekuwa Mbunge wa Mbinga Magharibi, sasa hivi jimbo jipya la Nyasa, marehemu Kapteni John Komba kwa kuhakikisha anapeleka maendeleo ya kweli kwa wananchi wake.
“Komba, aliwapenda wananchi wake kwa vitendo, nami nimekuja kuomba kura hapa Lituhi, Serikali yangu inathamini mchango wake kwa Taifa kwa kuleta maendeleo ya kweli,” alisema Dk. Magufuli.
Alisema anaomba urais huku akijua kuna changamoto kadhaa zinahitaji kutatuliwa kwa wakati.
“Awamu ya kwanza chini ya Mwalimu Julius Nyerere ilikuwa na kazi ya kuleta uhuru, mzee Mwinyi (awamu ya pili), alifungua milango ya biashara, awamu ya tatu mzee Mkapa aliweka mazingira sawa na awamu ya nne ya Jakaya Kikwete.
“Alichofanya kila mtu anashuhudia maendeleo ya nchi yetu, na sasa awamu ya tano ni Magufuli ninakuja kuleta mabadiliko katika Tanzania mpya,” alisema.
ARUSHA KOMBORA
Akiwa katika Jimbo la Peramiho, alirusha kombora na kusema wapo baadhi ya wanasiasa walikaa katika unaibu waziri kwa miaka 20 bila kupanda na walipoona mambo magumu wakakimbia ndani ya CCM.
“Ninawaomba mniletee Jenista Mhagama nifanye naye kazi, huyu ni mtiifu na mwaminifu ndiyo maana alipoteuliwa alikaa kwenye unaibu waziri kwa kipindi kifupi na kuteuliwa kuwa waziri kamili.
“Lakini wapo wengine wamekaa kwenye unaibu waziri kwa miaka 20 na mambo yalipowashinda wakahama na kwenda vyama vingine,” alisema bila kutaja jina la naibu waziri aliyehama.
Lakini hivi karibuni aliyekuwa Naibu Waziri wa Kazi na Ajira, Dk. Makongoro Mahanga, alitangaza kuihama CCM na kujiunga na Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema).
NCHIMBI: NCHI AIHITAJI MFANO WA RAIS
Mjini Songea, Mjumbe wa Kamati Kuu (CC) ya CCM, Dk. Emmanuel Nchimbi, aliuambia umati huo uliojitokeza kumsikiliza Dk. Magufuli, kwamba nchi inahitaji rais na sio mfano wa rais.
Alisema CCM imemteua Dk. Magufuli kuwa mgombea wake kwani ana sifa zote za kuiongoza nchi.
Dk. Nchimbi ambaye pia ni mbunge wa Songea Mjini anayemaliza muda wake alisema: “Mimi sijawahi kuwadanganya, nchi inahitaji rais na si mfano wa rais, na rais mwenyewe ni Dk. John Magufuli.”
Alisema akiwa mbunge wa Songea Mjini anayemaliza muda wake, amefanya kazi na Dk. Magufuli na ni mtu wa vitendo.
“Alikuja hapa akatuahidi barabara, imejengwa nanyi mmeona. Sasa tumchague Magufuli ni mtendaji, mchapakazi na muadilifu,” alisema Nchimbi kwenye mkutano huo uliofanyika Uwanja wa Majimaji.
0 comments:
Post a Comment