WAZIRI wa
Uchukuzi, Samuel Sitta alikaririwa juzi na vyombo vya habari, likiwemo gazeti
hili, kwamba ujenzi wa Reli ya Kati ambayo imekuwa ikisuasua kwa muda mrefu,
utaanza mwezi huu.
Alisema Rais
Jakaya Kikwete anatarajia kuweka jiwe la msingi Septemba 15 mwaka huu katika
eneo la Soga Mpiji wilayani Bagamoyo mkoa wa Pwani, kuanzisha ujenzi huo rasmi
utakaofanywa na Kampuni ya China Railway Construction.
Akasema
ujenzi huo utakaotumia miaka minne, utagharimu Sh trilioni 16. Waziri Sitta
alikumbusha kwamba mipango ya ujenzi wa reli hiyo, haijaanza sasa, bali ni
tangu wizara hiyo ilipokuwa chini ya Dk Harrison Mwakyembe, na kwamba mpango ni
kujenga reli ya kisasa itakayowezesha treni kusafiri kwa kilometa 120 kwa saa
na kubeba tani milioni 25 kwa mwaka.
Kadhalika,
Sitta alisema mbali ya mradi wa Reli ya Kati kutoka Dar es Salaam hadi Kigoma, ujenzi
wa Reli nyingine ya Kusini kutoka Mtwara kwenda Mbamba Bay, pia unatarajiwa
kufanyika.
Ingawa
Waziri Sitta aliyasema hayo akijaribu kuwaweka sawa Watanzania, baada ya
mgombea wa Chadema anayeungwa mkono na vyama vingine vinne kupitia Ukawa,
Edward Lowassa, kudai atajenga reli hiyo, akiwa amesahau kwamba tayari iko
kwenye mipango ya kujengwa, kwetu imekuwa ni habari njema.
Ni habari
njema kutokana na umuhimu wa reli hiyo ya kati kuwa na manufaa makubwa kwa nchi
yetu na imekuja wakati mwafaka, baada ya Serikali ya Awamu ya Nne, kujitahidi
katika ujenzi wa barabara nchini.
Mbali na
reli hiyo kuwa chachu ya nchi zinazotuzunguka, ambazo hazina bahari kuongeza
kupitisha mizigo katika nchi yetu na hivyo kukuza zaidi uchumi wetu, reli hiyo
pia itarahisisha usafirishaji wa abiria na bidhaa za hapa nchini.
Kwa sasa
bidhaa nyingi kutoka Dar es Salaam kwenda mikoa ya pembezoni kama Mara, Kigoma,
Kagera na hata Tabora, zinasafirishwa kwa njia ghali ya barabara na hivyo
zinapofika huko zinakuwa ghali pia.
Zipo taarifa
kwamba saruji ya kutoka Wazo Hill, Dar es Salaam au kutoka Mbeya inapofika mkoa
kama Mara, inakuwa juu kulinganisha na saruji inayotokea nchi jirani za Kenya
au Uganda na hii ni kutokana na usafiri ghali wa barabara.
Lakini, pia
kwenye vituo ambako reli inakopita, kama inafanya kazi kama ilivyokuwa miaka ya
sabini na themanini, inasababisha wananchi kufanya biashara kwa kutoa huduma
kwa abiria au wahudumu wa treni na hivyo kukuza uchumi wao pia.
Wakati
tukifurahia habari hii njema, tunawakumbusha pia wagombea, wasitoe ahadi ambazo
hazitekelezeki au zile ambazo tayari zimo kwenye mipango ya serikali eti kwa
lengo tu la kutafuta kura. Ni vyema wagombea wakatafiti hoja zao, kabla ya
kuzisema na kuhakikisha hoja wanazosema ni za kweli.
Ni matarajio
yetu kwamba kauli ya Waziri Sitta, itasimama kama alivyosema na ujenzi utaanza
na kumalizika katika kipindi hicho cha miaka minne. Kadhalika, tunaamini suala
la ujenzi wa Reli ya Kati na mengine yaliyo katika utaratibu wa kufanyiwa kazi
na serikali, hayatakuwa tena ‘mitaji’ ya kuombea kura.
0 comments:
Post a Comment