RAIS Jakaya
Kikwete ameeleza ndoto yake baada ya muda wake wa urais kumalizika, kuwa
ataanzisha taasisi ya maendeleo, itakayosimamia midahalo, semina na kongamano
kwa maendeleo ya taifa.
Pia,
ameeleza kuwa anatamani kukabidhi urais kwa mrithi wake wiki moja baada ya
matokeo kutangazwa.
Kikwete
amesema atakapostaafu ataishi kijijini kwao Msoga, Chalinze mkoani Pwani,
kuendeleza ufugaji na kilimo cha nanasi na hatapenda kujishughulisha kwa
kiwango kikubwa na masuala ya serikali.
Alisema hayo
Ikulu, Dar es Salaam jana, alipopokea Shahada ya Heshima kutoka Taasisi ya
Sayansi na Teknolojia ya Nelson Mandela.
Ndoto zake
Rais Kikwete
alisisitiza ndoto yake ni kuanzisha taasisi hiyo ya maendeleo, ambayo kazi yake
kubwa itakuwa kujadili, kupokea, kutafuta wadhamini na kushauri juu ya masuala
yatakayoiletea maendeleo nchi.
“Kuna watu
wamenishauri nianzishe taasisi ya kushughulikia migogoro, sitaki kabisa kuitwa
mchawi na wala taasisi hiyo siitaki kabisa, ila mgogoro ukitokea na
nikahitajika, basi nitachangia; Ila dhamira yangu ni kushughulikia masuala ya
maendeleo,” alisema.
Alitaja
baadhi ya masuala ya maendeleo yakayopewa kipaumbele na taasisi hiyo kuwa ni
pamoja na afya, afya ya akinamama na watoto, kilimo, maendeleo ya sayansi na
teknolojia na viwanda.
Maisha
kijijini
Alisema
atakapokabidhi madaraka kwa Serikali ya Awamu ya Tano, ataachana na shughuli za
kiserikali na badala yake ataenda kuishi kijijini, ambako ataendeleza shughuli
zake za ufugaji na kilimo.
“Kusema
ukweli nitakapostaafu sitopenda kujishughulisha sana na masuala ya kiserikali,
kwa sababu atakuwepo Rais mwingine lakini pia nitapenda nijishughulishe na
shughuli zangu nilime mananasi na kufuga. Ila nitajaribu kuchangia kwa kadri ya
uwezo wangu,” alisisitiza.
Rais Kikwete
alisema dhamira yake ni kukabidhi madaraka kwa Rais ajaye wiki moja baada ya
matokeo ya uchaguzi kutoka aweze kufungasha virago vyake na kwenda kijijini.
Wosia wake
Aidha, Rais
Kikwete alisisitiza juu ya umuhimu wa nchi kuendelea kusimamia na kukumbatia
maendeleo ya sayansi na teknolojia, nchi iweze kupiga hatua za maendeleo.
Akizungumzia
maendeleo ya Taasisi ya Nelson Mandela, alisema wazo la uanzishwaji wake katika
nchi za Afrika lilitokana na Benki ya Dunia kuziwezesha kupata maendeleo ya
haraka katika eneo la sayansi na teknolojia.
Alisema
benki hiyo ilihamasisha vyuo hivyo vianzishwe katika kanda nne ambazo ni za
Kaskazini, Kusini, Mashariki na Magharibi. Katika Kanda ya Kaskazini, Nigeria
imeanzisha chuo hicho Abuja na kwa Kanda ya Mashariki, kimeanzishwa Arusha.
“Tulipoanza,
tulikuwa hatuna fedha za kutosha, Benki ya Dunia ilihamasisha uanzishwaji wa
vyuo hivi, lakini haikufadhili uanzishwaji wake, lakini pia sisi tulitarajia
wenzetu wa jirani hasa wa Afrika Mashariki wanegtusaidia lakini walituachia
wenyewe,” alisema.
Alisema
Tanzania ilianzisha chuo hicho kutokana na umuhimu wake katika masuala ya
maendeleo. Alisema kwa sasa, tofauti ya maendeleo ya nchi zinazoendelea na
zilizoendelea kimaendeleo huonekana kutokana na hatua kubwa ambayo nchi
zilizoendelea imepiga katika sayansi na teknolojia.
Aliahidi
kushughulikia changamoto zinazokabili chuo hicho ikiwemo uhaba wa fedha.
Alisisitiza kwamba, Serikali kwa sasa kutokana na kukabiliwa na masuala makubwa
ikiwemo uchaguzi, ilishindwa kutoa kiasi cha fedha ilichoahidi kwa chuo hicho.
“Kuhusu ombi
lenu la kuandaa chakula kwa ajili ya wafadhili mliowaalika katika harambee ya
kuchagia mfuko wenu maalumu kuendeshea chuo, muda mliopanga nitakuwa
nimeshastaafu, hivyo nitawaandikia barua hao wafadhili na baadaye kulikabidhi
jambo hili kwa Rais ajaye,” alisema.
Mwenyekiti
wa Baraza la Taasisi ya Nelson Maendela cha Sayansi na Teknolojia, Profesa
David Mwakyusa, alisema wamemtunuku Kikwete shahada hiyo, kutokana na kutambua
mchango wake katika masuala ya elimu hasa eneo la sayansi na teknolojia.
“Tulipanga
Shahada ya Kwanza tumpatie Rais Kikwete kutokana na kujitoa kwake katika mambo
ya sayansi na teknolojia,” alisema.
Alisema
pamoja na chuo hicho kuanzishwa na kuanza kufanya vizuri, bado kinakabiliwa na
changamoto mbalimbali za kukiendeleza ikiwemo uhaba wa fedha.
Kwa mujibu
wa Profesa Mwakyusa, Serikali iliahidi kuipatia taasisi Sh bilioni 7.2 lakini
hadi sasa kimepatiwa Sh bilioni mbili.
Alisema kwa
sasa umeanzishwa mfumo maalumu wa kuendesha chuo hicho na imeandaliwa harambee
kwa ajili ya wafadhili.
“Tunakuomba
mheshimwia Rais utusaidie kuwaalika wale wafadhili, ambao sisi tumewabaini na
tunaona wataweza kutusaidia angalau tupate hasa dola za Marekani milioni 10,”
alisema.
0 comments:
Post a Comment