SEKTA ya Utalii ni muhimu katika ukuaji wa uchumi nchini kwa
kuwa inachangia kuliingizia Taifa fedha za kigeni.
Utalii unategemea uwepo wa maliasili na vivutio ili kuwavutia
wageni kuja kutembea kufurahia ama kujifunza mambo mbalimbali yanayopatikana
Tanzania. Kwa kutambua umuhimu wa sekta ya utalii, mwandishi wa makala haya
amefanya mahojiano na Mkurugenzi Msaidizi Idara ya Utalii, Uzeeli Kiangi na
kueleza hali ya utalii nchini na mchango wake katika ukuaji wa uchumi wa
Tanzania.
Kiangi anasema Tanzania ni moja ya nchi chache duniani
zilizojaliwa kuwa na vivutio vingi vya utalii ikiwemo mbuga za wanyama, mito na
mabonde ya kuvutia pamoja na maajabu mengine. Anasema Tanzania ni nchi pekee
ambayo zaidi ya asilimia 25 ya nchi kavu ni eneo lenye misitu ya hifadhi za
wanyamapori pamoja na maeneo ya mapori ya akiba yaliyotengwa na serikali.
Kiongozi huyo anasema, moja ya vivutio vikubwa ni hifadhi ya
wanyama ya Serengeti, Bonde la Ngorongoro , Ziwa Manyara pamoja na mlima mrefu
kuliko yote barani Afrika, Mlima Kilimanjaro. Vivutio vingine ni pamoja na
hifadhi za wanyama za Mikumi, Ruaha na Selous ambazo kila moja ina wanyama au
miti ambayo ni adimu na inapatikana Tanzania pekee. Kiangi anasema utalii
umegawanyika katika sehemu kuu mbili ambazo ni utalii wa ndani na utalii wa
nje.
Utalii wa ndani ni ule ambao Watanzania wanatembelea maeneo
tofauti na pale wanapoishi au kutembelea hifadhi na vivutio vingine
vinavyopatikana nchini. Utalii huu hujumuisha mapumziko ya familia hasa wakati
wa likizo katika moja ya hifadhi za taifa au maeneo mengine ya utalii
yanayopatikana ndani ya nchi pamoja na utalii wa kimasomo. Utalii wa nje
unahusisha watalii ambao wanasafiri kutoka nchi mbalimbali na kuja Tanzania kwa
ajili ya kupumzika wakati wa likizo, utalii wa masomo na kufanya tafiti pamoja
utalii wa kuja kujionea wanyama na vitu vingine visivyopatikana katika maeneo
yao.
Kwa mujibu wa Kiangi, watalii wanaotoka nje ya nchi kuja
Tanzania ni wengi kuliko wale wa ndani. Anasema watalii wa kutoka nje ya
Tanzania wamekuwa wakiongezeka mwaka hadi mwaka kutoka watalii 295,312 mwaka
1995 hadi kufikia watalii 1,140,156 mwaka 2014. Ukuaji wa utalii hadi kufikia
mwaka jana 2014, umesaidia kuongeza kasi ya ukuaji wa uchumi na kusaidia juhudi
za serikali katika kuleta maendeleo kwa wananchi.
Ongezeko hili la watalii limesaidia kuongeza upatikanaji wa
fedha za kigeni kutoka dola milioni 259.44 mwaka 1995 sawa na Sh milioni
155,663 hadi kufikia dola milioni 2,006.32 sawa na Sh milioni 3,316,647.59
mwaka 2014. Kiangi anasema, watalii wengi hufika nchini kwa kutumia zaidi
usafiri wa anga. Mwaka jana watalii 636,107 walitumia usafiri huo na watalii
439,421 walifika kwa kutumia usafiri wa barabara.
Aina nyingine ya usafiri inayotumika ni usafiri wa maji.
Mwaka jana watalii 59,999 waliingia nchini kwa kutumia usafiri huo na wengine
wapatao 4,629 waliingia kwa kutumia usafiri wa reli. Anasema, watalii wengi
hufika nchini kwa sababu ili kupumzika wakati wa likizo kazini. Kwa mujibu wa
Kiangi, mwaka 2014 watalii 920,028 walifika kwa ajili ya mapumziko. Mwaka jana
watalii 85,818 wanafika kwa ajili ya kutembelea marafiki, ndugu na jamaa zao wa
karibu, 68,341 wanafika kwa ajili ya shughuli za kibiashara na mafunzo ya
kitaalamu.
Pamoja na ukuaji huo wa utalii, Kiangi anasema bado utalii wa
ndani haujawa na hamasa kubwa kama ulivyo utalii wa nje kutokana na kuwepo na
idadi ndogo ya Watanzania wanaojihusisha na utalii wa kutembelea vivutio
vilivyopo nchini. Kiangi anasema, utalii wa ndani unakua taratibu kwa kuwa
wananchi wengi wanaogopa gharama kubwa za chakula, malazi na usafiri.
Anasema, serikali itaanzisha usafiri maalum pamoja na
kuwekeza kwenye hoteli zitakazotoa huduma nafuu ya chakula na malazi katika
hifadhi za taifa ili kukuza utalii wa ndani. Kiangi anasema, serikali itawekeza
kwenye hoteli zitakazotoa huduma ya chakula kwa bei ndogo ambazo kila mwananchi
ataweza kuimudu. Katika juhudi za kuhakikisha kuwa utalii wa ndani unakua,
Shirika la Hifadhi za Taifa Tanzania (TANAPA) hivi karibuni linatoa wito kwa
wananchi kutembelea hifadhi za taifa ili waweze kunufaika kwa kujionea vivutio
pamoja na kupata zawadi maalumu.
Kampeni ya uhamasishaji utalii wa ndani ni moja ya hatua
muafaka zinazochukuliwa na serikali kwa kushirikiana na wadau ili kuongeza
idadi ya Watanzania wanaotembelea hifadhi za taifa na kuongeza mapato kupitia
utalii. Mkurugenzi wa Utalii na Masoko kutoka TANAPA, Ibrahim Mussa anasema,
utalii wa ndani umeongezeka lakini kwa idadi ndogo ukilinganisha na watalii
kutoka nje ya nchi.
Mussa anasema, utalii wa ndani ni rasilimali kubwa lakini
bado Watanzania wana mwitikio mdogo katika jambo hilo. Anasema, TANAPA imeanzisha
kampeni ya kuhamasisha wananchi kutembelea hifadhi za taifa kwa kipindi cha
miezi sita kuanzia Julai hadi Desemba mwaka huu. Mussa anasema, kutakuwa na
usafiri kuwapeleka wananchi hadi hifadhi za taifa ikiwa ni njia mojawapo ya
kupunguza gharama pamoja na kutoa huduma ya chakula na malazi kwa bei nafuu
kwenye hoteli za kitanzania zijulikanazo kama Mabanda lakini zenye huduma nzuri
na nafuu.
Anasema, huduma hiyo ya mabanda itawawezesha wananchi kupata
huduma ya malazi kwa bei ya chini kuanzia Sh 15,000 hadi 80,000 kitu ambacho
wananchi wengi wanaweza kumudu. Mussa anasema, mwaka jana idadi ya watalii wa
ndani imeongezeka hadi kufikia laki nne na nusu hivyo kuonesha kuwa endapo
juhudi zaidi zitafanyika kuhamasisha wananchi kutembelea hifadhi za taifa, wananchi
wengi zaidi wataenda kutalii.
Ili kuhifadhi vivutio vilivyopo, Wizara ya Maliasili na
Utalii kwa kushirikiana na wadau ikiwemo Wakala wa Taifa wa Misitu watasaidia
kulinda na kurejesha madhari rafiki kwa ajili ya ukuaji wa utalii. Wakala hiyo
imesaidia upandaji wa miti kwenye eneo la hekta 40,000 katika mashamba 18 nchi
nzima na kufikisha jumla ya hekta 96,500 zilizopandwa nchini na kupunguza hali
ya jangwa iliyokuwa ikiongezeka kila mwaka.
Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Taifa wa Misitu, Juma Mgoo
anasema, wamepata mafanikio ikiwemo kufanikisha upandaji wa miti na kuokoa
baadhi ya misitu iliyokuwa hatarini kutoweka. Mgoo anasema, wamefanikisha
kuingiza Sh bilioni 85.3 kwenye pato la taifa kwa mwaka 2014/2015 ikiwa ni
ongezeko kubwa ukilinganisha na Sh bilioni 39 walizochangia kwenye bajeti ya
mwaka 2010.
Anasema, wameweza kupima na kuweka mipaka ya misitu ya taifa
102 ambayo ni sawa na asilimia 25 ya misitu yote 455 ya hifadhi iliyopo nchini.
Mgoo anasema wanajivunia kuona utalii unazidi kukua na hivyo ni wajibu wa
wananchi kuhifadhi na kutunza misitu ili iweze kusaidia kuvutia watalii pamoja
na kuongeza pato la taifa.
Kiangi anasema, ujangili ni miongoni mwa mambo yanayoathiri
sekta ya utalii na kwamba, madhara yake hayawezi kuonekana moja kwa moja hivi
sasa. Kwa mujibu wa Kiangi, madhara ya uovu huo yataanza kuonekana baadaye
hivyo ni wajibu wa kila mtu kuhakikisha analinda rasilimali za utalii
zisipotee. Anasema jukumu la kulinda na kuhifadhi rasilimali za utalii na nchi
kwa ujumla si la serikali peke yake.
0 comments:
Post a Comment