MSAJILI
wa Vyama vya Siasa nchini, Jaji Francis Mutungi ameviagiza vyama vya siasa
kudhibiti vitendo vya wanachama wake vinavyoweza kusababisha uvunjifu wa amani,
ikiwamo tabia iliyojitokeza ya baadhi ya wanachama na mashabiki wa vyama hivyo
kuwazomea na hata kuwarushia mawe wanachama na mashabiki wa vyama vingine, hasa
pale wanapovaa sare za vyama vyao.
Amesema
vyama vya siasa vina wajibu wa kijamii na kisheria wa kudhibiti vitendo hivyo.
Katika taarifa yake kwa umma jana, Jaji Mutungi alisema amevitaka na kuviagiza
vyama vyote vya siasa, kutoa maelekezo kwa wanachama wake wote na kuwataka wawe
na utulivu katika kipindi chote cha Uchaguzi kwa kuheshimu sheria na kuzingatia
dhana ya kufanya siasa za kistaarabu ikijumuisha kuwa na uvumilivu wa kisiasa.
“Siku
za hivi karibuni kumejitokeza tabia ya baadhi ya wanachama na mashabiki wa
baadhi ya vyama vya siasa kuwazomea na hata kuwarushia mawe wanachama na
mashabiki wa vyama vingine na hasa pale wanapovaa sare za vyama vyao,” alisema
Jaji Mutungi.
Jaji
Mutungi alisema katika kipindi cha uchaguzi ni kipindi ambacho kuna ushindani
mkubwa na matukio mengi ya kisiasa, hali ambayo inahitaji vyama vya siasa
kuzingatia sana utii wa sheria za nchi na kufanya siasa za kistaarabu, ili
kujiepusha na vitendo/matendo yanayoashiria uvunjifu wa amani.
Pia
alisema anaamini kuwa migongano na migogoro baina ya vyama vya siasa au baina
ya vyama vya siasa na wadau wengine wa uchaguzi. “Navitaka na kuviagiza vyama
vyote vya siasa kutoa maelekezo kwa wanachama wake wote na kuwataka wawe na
utulivu katika kipindi chote cha Uchaguzi kwa kuheshimu Sheria na kuzingatia
dhana ya kufanya siasa za kistaarabu ikijumuisha kuwa na uvumilivu wa kisiasa,”
alisema Msajili wa Vyama vya Siasa.
“Nawasihi
wadau wengine wote ambao ni wapenzi wa demokrasia ya vyama vingi vya siasa na
ambao wangependa kuona nchi yetu ikimaliza kipindi hiki cha Uchaguzi kwa amani,
basi wasisite kutoa taarifa kwa mamlaka husika punde wanapoona mfuasi,
mwanachama au kiongozi wa chama anafanya vitendo vya ukiukwaji wa sheria
kuhusiana na masuala ya kisiasa na uchaguzi.”
Kauli
ya Jaji Mutungi imekuja huku Polisi wa Kanda ya Dar es Salaam wakitoa onyo kwa
watu wanaojihusisha na vitendo vya kuzomea waliovalia sare za vyama na kusema
hatua za kisheria zitachukuliwa dhidi yao.
Kamanda
wa Polisi wa Kanda ya Dar es Salaam, Suleiman Kova, alizungumzia vitendo hivyo
vya kuzomea na kusema, kinachofanyika sasa, ni kufuatilia baadhi ya picha
zilizosambaa kwenye mitandao zikionesha matukio hayo, kubaini wahusika
wafikishwe kwenye vyombo vya sheria.
Picha hizo zilionesha baadhi ya watu walio waliovalia
sare za chama kimoja cha siasa, wakizomewa na umati wa vijana ingawa
haikufahamika mara moja, eneo ambako vitendo hivyo vilifanyika. Kamanda Kova
alisema mtu yeyote anayo haki ya kuvaa nguo ya rangi yoyote bila kubughudhiwa.
Kuhusu
kampeni, Kova alihimiza wanasiasa kufanya kampeni za amani na kuasa viongozi wa
vyama vya siasa kuendesha kampeni za kistaarabu pamoja na kuonya wafuasi wao
wanapokwenda kinyume.
Kwa
mujibu wa Kova, katika baadhi ya vyama, kunadaiwa kuundwa makundi ya ushabiki
yanayolenga kuleta vurugu kwenye mikutano ya vyama pinzani. Viongozi wa dini na
siasa Katika hatua nyingine, Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) imewakumbusha
viongozi wa dini nchini kutoonesha hisia za kisiasa na kuepuka kushawishi
waumini wao kuegemea upande wowote wa chama au mgombea katika kampeni
zinazoanza kesho.
Hayo
yalisemwa na Mwenyekiti wa NEC, Jaji mstaafu Damiani Lubuva wakati wa mkutano
kati ya Tume na viongozi wa dini katika kuwaelezea maandalizi ya uchaguzi mkuu
wa Oktoba 25, mwaka huu.
Jaji
Lubuva aliwataka viongozi hao wanapotoa mafundisho ya uchaguzi kutoonesha hisia
kwa upande wowote wa chama cha siasa na zaidi kuepuka kuwashawishi waumini
kuegemea upande wowote wa chama au mgombea.
Alisema
viongozi wa dini wanao wajibu wa kutumia majukwaa yao kuelimisha na kufahamisha
wapiga kura ili waweze kufanya maamuzi baada ya kupata taarifa sahihi na si
kuruhusu wanasiasa kuyatumia majukwaa hayo ya dini kufanyia kampeni.
Alisema
sheria za uchaguzi zinakataza viongozi wa dini kutumika katika masuala ya
kisiasa kama vile kufanya kampeni za uchaguzi katika maeneo ya ibada.
Mkurugenzi wa Uchaguzi wa NEC, Kailima Ramadhani alisema jana kuwa, Tume
haijatoa ratiba ya kampeni kutokana na baadhi ya vyama kutopeleka rasimu ratiba
ya kampeni.
Alisema
ni vyama vitatu ndiyo vilivyowasilisha ratiba, ikiwemo CCM inayozindua kampeni
zake Jumapili jijini Dar es Salaam. Chadema haijatangaza siku ya kuzindua
kampeni zao.
0 comments:
Post a Comment