Mikoani. Siku chache baada ya vyama vinavyounda Ukawa kutangaza
mgawanyo wa majimbo, baadhi ya majimbo hayo yamekumbwa na sintofahamu baada ya
wanachama kutokubaliana na uamuzi ya viongozi wa kuachiana majimbo.
Vyama
vinavyounda Ukawa; Chadema, NCCR-Mageuzi, CUF na NLD vimekubaliana kusimamisha
mgombea mmoja wa kuanzia ngazi ya urais hadi udiwani kwa kuangalia, pamoja na
mambo mengine, chama chenye nguvu kwenye jimbo husika na kura za uchaguzi wa
mwaka 2010.
Tayari
Chadema na CUF vimeshatoa orodha ya majimbo vitakavyosimamisha wagombea wake na
kuacha baadhi, ambayo yameibuka kutoelewana baina ya uongozi wa juu na wa
wilaya.
Moja ya
majimbo ambayo hayakuwekwa kwenye orodha ya mgawanyo ya Chadema iliyotolewa
mapema wiki hii ni Ngara ambayo iliachiwa NCCR-Mageuzi, lakini uongozi wa
wilaya wa chama hicho kikuu cha upinzani umesema utasimamisha mgombea.
Mwenyekiti
wa Chadema wilayani Ngara, Kennedy Staford amesema Kamati Kuu ya Ukawa
imewachanganya wananchi wa jimbo hilo kutokana na uamuzi huo wa kuipa
NCCR-Mageuzi nafasi ya kusimamisha mgombea.
Staford
alisema kitendo cha kuipa jimbo hilo NCCR-Mageuzi bila viongozi wa wilaya
kushirikishwa ni kuwakatisha tamaa wanachama kuendelea kuunga mkono Ukawa
kupitia Chadema.
Alisema
chama kilichopendekezwa kusimamisha mgombea hakina wanachama na wafuasi
wanaoweza kutoa ushindani kwa mgombea wa CCM. “Jimbo la Ngara tulishafanya
mchakato wa kumpata mgombea aliyepigiwa kura za maoni na tayari amechukua fomu
ya kuwania jimbo kupitia chama chetu,” alisema Staford.
Majimbo
yaliyotangazwa na Chadema kusimamisha mgombea katika Mkoa wa Kagera ni pamoja
na Karagwe, Kyerwa, Bukoba Mjini, Muleba Kaskazini, Biharamulo na Muleba
Kusini.
Wakati
hayo yakitokea Ngara, Ukawa wilayani Kakonko pia imeingia katika mvutano baada
ya baadhi ya vyama shirika kuweka wagombea wake kuwania ubunge kwa Jimbo la
Buyungu na kukiuka makubaliano. Hali hiyo imejitokeza baada ya Samso Bilago
kuchukua fomu ya kuwania ubunge kwa tiketi ya Chadema na kusababisha wasiwasi
kwa wananchi kutokana na jimbo hilo kuachwa kwa NCCR-Mageuzi ambayo mgombea
wake Mawazo Atanasi pia amechukua fomu.
Akizungumzia
hali hiyo, katibu wa CUF jimboni humo, Odasi Kalimanzila alisema msimamo wa
Ukawa haujavunjika licha ya kwamba kuna baadhi ya vyama ambavyo vimeonekana
kwenda kinyume na makubaliano. Hata hivyo, katibu wa NCCR-Mageuzi wilayani
Kakonko, Marco Bajora alisema bado kuna changamoto kubwa katika umoja huo, na
kwamba wanachosubiri ni uamuzi wa wananchi kumchagua kiongozi atakayefaa katika
kuleta maendeleo.
Ester
Bulaya azua balaa
Wakati
huohuo, aliyekuwa mshindi wa kura za maoni Bunda Mjini wa Chadema, Pius Masururi
ametangaza kukihama chama hicho na kujiunga CCM huku mwenyekiti wa jimbo hilo,
Samuel Imanani na wanachama 50 wakiwamo viongozi wakijivua uanachama.
Masururi,
aliyepata kura 65 mbele ya wapinzani wake wa karibu, Magembe Makoye (40) na
Ester Bulaya (37) katika kura za maoni zilizopigwa Julai 29 mwaka huu,
ametangaza uamuzi wake huo jana kupitia kituo cha redio cha Mazingira FM cha
mjini Bunda.
Masururi
amesema ameamua kukihama chama hicho baada ya kutofurahiswa na kitendo cha
Kamati Kuu ya Chadema kupuuza uamuzi wa wanachama kwa kukata jina la
aliyeshinda kura za maoni.
Katika
jimbo la Bunda Mjini, Chadema imebadilisha matokeo na kumteua mshindi wa tatu,
Ester Bulaya kupeperusha bendera ya chama hicho, jambo lililowaudhi baadhi ya
makada wake.
Baadhi
ya wanachama walioongozwa na mwenyekiti wa jimbo hilo, Samuel Imanani wamesema
kitendo cha makao makuu ya Chadema kutengua uamuzi wa kura zao za maoni ni
udhalilishaji mkubwa, hivyo hawana budi kukihama chama hicho. “Tumeamua
kuuachia uongozi wa makao makuu uendeshe mambo yote, nasi tusiwe tena wanachama
maana hautusikilizwi,” alisema Mashaka Kipili mmoja wa wanachama hao.
Katika
tukio jingine, aliyekuwa mbunge Mbarali kupitia CCM, Dickson Kilufi amekumbana
na vikwazo kwenye chama chake kipya cha Chadema baada ya uongozi wa
wilaya kusema hauna taarifa za kutaka agombee ubunge wa jimbo hilo.
Mwenyekiti
wa Chadema wilayani Mbarali, Peter Mwashiti alisema taarifa za Kilufi kujiunga
Chadema anazisikia kwenye vyombo vya habari na mitaani na kwamba suala la
kutaka agombee ubunge halipo kwa vile tayari alishapitishwa Liberatus
Mwang’ombe kuwa mgombea wa jimbo hilo.
‘‘Kama
amejiunga na Chadema, tunamkaribisha, lakini kibaya ni kwamba hajawahi
kuwasiliana na kiongozi yeyote wa Chadema Wilaya ya Mbarali na cha
kushangaza tunasikia ameanza kujitangaza eti kateuliwa kugombea ubunge kwa
tiketi ya Chadema. Sisi tuna mgombea wetu na ameshachukua fomu pale
halmashauri,” alisema.
Kilufi
alipoulizwa kuhusu hoja hizo, alisema aliteuliwa na viongozi wa kitaifa wa
Chadema kupeperusha bendera ya chama hicho kwenye ubunge wa Jimbo la Mbarali.
Wakati
mgogoro huo ukiendelea, mwenyekiti wa CCM Mbarali, Mathayo Mwangomo amesema
Kilufi alikuwa mzigo ndani ya chama hicho hivyo wanashukuru kujiengua kwake na
kujiunga na Chadema.
Pia,
Kilufi alijitetea kuwa hakuwa mzigo, bali mzigo ni viongozi wa CCM ambao
alidai wanapenda rushwa.
Wafuasi
wa Chadema, Kata ya Forest Mbeya waliandamana hadi katika ofisi za wilaya
za chama hicho wakipinga shinikizo la uongozi wao kutaka aliyekuwa diwani, Boyd
Mwabulanga achukue fomu za kuwania tena nafasi hiyo.
Mwanachama
wa chama hicho aliyejitambulisha kwa jina la Mwamakamba, alisema anashangazwa
na kitendo cha baadhi ya viongozi kutumia mbinu za kiujanja ujanja kutaka
Mwabulanga agombee tena badala ya Henry Mwakikambu aliyeshinda kura za maoni.
Viongozi
wa wilaya walilazimika kuwatuliza wandamanaji hao kwa kuwaeleza kwamba kaimu
katibu mkuu wa Chadema, John Mnyika aliruhusu Mwakikambaku achukue fomu
haraka na kuapishwa mahakamani ili agombeee nafasi hiyo. Pia, katika Jimbo la
Handeni Mjini vyama vya CUF na Chadema vimesimamisha wagombea ubunge licha ya
mgawanyo wa majimbo hayo kuonyesha kuwa CUF ndiyo kimeachiwa nafasi hiyo.
Katibu
wa Chadema Jimbo la Handeni Mjini, Zaharia Yohana alisema ni kweli
wamesimamisha wagombea ubunge na udiwani katika majimbo yote pamoja na kata
zote Handeni Mjini na Vijijini ili kushiriki uchaguzi mkuu.
Kuhusu
mchakato huo kukiuka makubaliano ya vikao vya Ukawa, alisema hawezi
kulizungumzia hilo bali anafuata maelekezo ya viongozi wake.(Startv leo)
0 comments:
Post a Comment