UTAFITI na ubunifu vina nafasi kubwa katika kulinufaisha
taifa, hasa ikizingatiwa kuwa hakuna nchi duniani inayoendelea bila kuzingatia
ubunifu hasa kwenye masuala ya sayansi na teknolojia.
Tume ya Sayansi na Teknolojia (Costech) iliyopo chini ya
Wizara ya Mawasiliano, Sayansi na Teknolojia kwa kushirikiana na wahisani
wamejikita katika kusaidia vijana walioonesha uwezo wa kubuni miradi ya
maendeleo. Kituo cha Kuendeleza Teknolojia ya Habari na Mawasiliano kiitwacho
DTBi cha tume hiyo ni msaada mkubwa kwa vijana wabunifu katika tehama.
Mkuu wa Utawala na Fedha wa kituo hicho, Makange Mramba
anasema, lengo la kuanzisha kituo hicho ni kusaidia vijana wajasiriamali wa
Tehama wenye ubunifu wa aina mbalimbali kuanzisha kampuni zao na wenye kampuni
kusaidiwa ili zikue na kuchangia katika pato la taifa.
“DTBi tunawasaidia vijana waanzishe kampuni na wale ambao
tayari wanazo basi kampuni zao ziweze kukua waweze kuchangia pato la Serikali
kwa maana ya kulipa kodi na pia waweze kuajiri wenzao na pia kutoa ufumbuzi wa
matatizo ambayo yanazikabili sekta zetu mbalimbali kama kilimo, madini, afya na
nyinginezo,” anasema Mramba. Anasema katika kufanya hivyo, wizara kwa
kushirikiana na wadhamini walikubaliana kianzishwe kituo chini ya mwavuli wa Costech
Juni 2011.
Mramba anasema, baada ya kuanzishwa kituo hicho, kazi ya
kwanza ilikuwa ni kuelimisha wajasiriamali kujitokeza wakiwemo waliokuwa vyuoni
wakitengeneza programu lakini wanakumbana na changamoto mbalimbali ikiwa ni
pamoja na upatikanaji wa mitaji, eneo la kufanyia kazi na pia elimu ya
ujasiriamali. Anasema DTBi wana mfumo wa kutatua matatizo ya wajasiriamali
wabunifu katika hatua ya mwanzo kwa kuwaunganisha na mitaji, kuwatambulisha
sokoni na kuwapa ushauri kwa kuwa ni vijana wadogo wanaohitaji malezi na msaada
wa kiteknolojia.
“Wengine wanahitaji msaada wa kiteknolojia, anaweza kuwa
anajua jambo fulani lakini kuna ujuzi ambao hana ili atimize jambo analotaka
kufanya kwa hiyo sisi tunawaunganisha na wataalamu ili waweze kusaidiwa
kukamilisha jambo lao na wengine wanakuja na mawazo mazuri lakini wao sio
wanateknolojia kwa hiyo tunawaundia timu ya wataalamu,” anasema Mramba.
Anasema kituo hicho kimeweza kujiimarisha na sasa watu
wanakifahamu vizuri na kuna vijana waliojengwa na kituo hicho akitolea mfano wa
MaxMalipo. “Ukinunua umeme, muda wa maongezi, ukilipia leseni ya gari kulipia
malipo yoyote kwa kupitia MaxiMalipo unatumia huduma inayotokana na zao letu,
tunda jingine ni Day One ambaye ametengeneza mfumo unaotumika na halmashauri
mbalimbali kukusanya kodi,” anasema Mramba.
Anasema vijana wanakaa katika kituo hicho wakifundishwa
biashara na pia teknolojia kwa miaka mitatu na baada ya hapo wanakuwa
wameshakomaa, wanajitegemea huku wakiendelea kupokea ushauri. Mramba anasema,
Day One imetoa msaada mkubwa katika kuwatambua walipa kodi na kuwaingiza katika
mfumo wa malipo katika halmashauri 15 zikiwemo za Temeke, Arusha na Moshi.
Anasema, kampuni hizo pia zimeweza kuzalisha nafasi za ajira kwa vijana
waliokuwa wakihangaika mtaani.
Mramba anasema, kuna vijana wanatoka vyuoni moja kwa moja nao
wanakubaliwa kujiunga kwenye kituo hicho na anatoa mfano wa kijana aliyeweza
kutengeneza mfumo unaosaidia katika tatizo la wizi wa simu. Kijana huyo hivi
karibuni ataingia mkataba na kampuni ya simu za mkononi ili mfumo huo uanze
kutumika. Mfumo huo ni wa kulinda simu za mkononi za smart phone.
“Imekuwa ni vigumu sana unapoibiwa simu kupata taarifa zao
zilizokuwa ndani ya simu lakini mfumo huo una uwezo wa baada ya kuibiwa simu, ukipata
simu nyingine unaita taarifa zako zote zinakuja. “Baada ya kuibiwa simu yako,
ukishapata simu nyingine unaingiza namba ya siri basi unaita taarifa zako zote
zinakuja, ikiwa ni pamoja na namba za simu na picha.
Mfumo huu hivi karibuni utakuwa sokoni,”anasema Mramba.
Anasema mfumo una uboreshwaji wa vitu ambavyo havipatikani katika mifumo
mingine ya aina hiyo na kwamba, unaweza kuendelea kumfatilia mtu aliyechukua
simu hiyo, kumtumia ujumbe mara kwa mara na pia hatakuwa na uwezo wa kuitumia
wala kuifuta (flash) vitu vilivyopo kwenye simu hivyo atalazimika kuirudisha.
Mramba anasema, pia vijana walioko katika kituo hicho
wameweza kutengeneza mfumo wenye uwezo wa kufuatilia, kwa mfano, mmiliki wa
pikipiki za biashara maarufu kwa jina la bodaboda anaweza kutumia simu yake na
pia unaweza kuizima boda boda hiyo kama anaona inaelekea sehemu ambayo
huielewi. Kwa mujibu wa Mramba, kuna programu nyingine inayoweza kusaidia mtu
kuona teksi iliyoko jirani na alipo kama anahitaji huduma hiyo hivyo badala ya
kumpigia dereva aliye mbali na hapo atamwita aliye karibu.
“Programu hii pia itakuonesha teksi inayopita karibu na wewe
namba yake ya simu, historia ya teksi hiyo pamoja na maelezo ya dereva
husika... unaweza kuona kama imewahi kupata ajali au la, uzoefu wa dereva, na
hii yote ni kwa kutumia simu yako ya mkononi,” anasema Mramba. Programu hiyo
itaunganisha mfumo wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) pamoja na taarifa za
Jeshi la Polisi na Kikosi cha Usalama Barabarani kwa ajili ya kupata taarifa na
kuziunganisha kwa programu hiyo ambayo iko katika hatua ya kuiendeleza.
Anasema lengo la DTBi ni kutumia mfumo wa Tehama kutatua
matatizo ya watu ambayo hadi sasa hayana suluhisho. “Sasa tunaandaa pia
programu ya kuangalia televisheni kupitia simu ya mkononi ambazo ni smart
phone, inaweza kukamata vituo vyote vya televisheni ukiwa popote huna haja ya
kukimbia nyumbani kuangalia taarifa ya habari au kipindi chochote,” anasema
Mramba.
Mramba anasema kituo hicho kinatafuta uwezekano wa kupanua
wigo wa huduma ili kuwanufaisha watu wengi zaidi kwa kuwapata wabunifu wengine
ambao wako katika mikoa mingine. Kwa sasa kituo hicho kinachukua vijana kutoka
vyuo vikuu kadhaa ikiwa ni pamoja na Chuo Kikuu cha Dodoma (UDOM). Mramba
anasema kituo hicho kinakabiliwa na changamoto ikiwa ni pamoja na wajasiriamali
kutokuwa na mwamko wa kutumia fursa kama hizo.
“Wengine wanahangaika huko pembeni, pamoja na matangazo
tunayotoa lakini hawajitokezi inabidi tuwatafute,” anasema Mramba. Anasema
vijana wengi hawana mwamko wa kuwa wajasiriamali, wengi wao wanakimbilia
kutafuta kazi baada ya kumaliza masomo yao badala ya kufikiria kujiajiri. “Hata
wale wanaoweza kuwa wabunifu wazuri sana na kusaidia nchi wanakimbilia kupata
ajira ambazo hazipo,”anasema Mramba.
Anataja changamoto nyingine kuwa ni kuingiza sokoni utaalamu
walioubuni kwa sababu imeshajengeka imani kwamba teknolojia lazima itoke katika
nchi zilizoendelea. Mramba anasema, bado watu hawaamini kwamba watu
wanaowafahamu wanaweza kuja na jambo linaloweza kusaidia dunia. Kwa mujibu wa
Mramba, mitaji ni moja ya changamoto kwa kuwa taasisi nyingi za fedha ikiwa ni
pamoja na benki hawatoi mikopo kwa wabunifu hao kutokana na asili ya kazi zao
ambazo zinachukua muda mrefu kuanza kurudisha fedha.
“Teknolojia zetu ukiwekeza mwaka huu unatarajia kuanza kuvuna
baada ya miaka mitatu au minne, afanyie majaribio, apeleke sokoni ikafanyiwe
majaribio na kukubaliwa na kuingia sokoni hii inachukua muda mrefu kwa hiyo
huwezi kumpa mkopo ukamwambia aanze kulipa mwezi ujao,” anasema. Mramba
anasema, unahitajika mfumo wa kuwatambua wabunifu hao ili wapewe muda wa
kutosha kuanza kupata faida na kurejesha mkopo.
Anasema, Serikali pia inapaswa kutoa nafasi kwa wabunifu
wanapokuja na teknolojia waweze kujaribu kwenye taasisi za serikalini au
kwingineko inakohitajika. Mramba anasema, sheria na taratibu za sasa
haziwaruhusu wabunifu kufanya hivyo.
0 comments:
Post a Comment