KARIBU robo
tatu ya viongozi wakuu wa Chadema wilayani hapa, walijiuzulu nyadhifa zao jana
na kutangaza kuhamishia nguvu zao kwa mgombea ubunge wa CCM, Stephen Wasira.
Wamedai
wanafanya hivyo kutokana na kukerwa na kitendo cha makao makuu ya Chadema,
kumpitisha Esther Bulaya kuwa mgombea ubunge jimboni humo, licha ya kuwa
alishika nafasi ya tatu katika kura za maoni.
Bulaya
aliyekuwa Mbunge wa Viti Maalumu (CCM), alihamia Chadema hivi karibuni na moja
kwa moja kwenda kujaribu siasa za majimbo, akianzia Bunda kwa tiketi ya chama
chake kipya.
Aidha,
aliyekuwa mshindi katika kura za maoni, lakini akaondolewa na vikao vya chama,
Pius Masururi, pia ametangaza kuhamia CCM. Waliojiengua Chadema na kundi kubwa
la wanachama ni Mwenyekiti wa jimbo hilo, Samuel Alfred, Katibu Mwenezi wake,
Emmanuel Malibwa na Katibu wa Chadema wilayani Bunda, Rita Itandilo.
Wakizungumza
jana katika Hoteli ya Green Garuden mjini hapa, viongozi hao walisema wameamua
kujivua nyadhifa zao ili wabaki wanachama wa kawaida kwa kuwa viongozi wao wa
Mkoa, Kanda na Taifa wamekiuka Katiba ya chama hicho.
“Kwa
kile kilichotokea kupitia uongozi wetu wa mkoa, kupitia Katibu wetu wa Chama
Mkoa Chacha Heche na Mwenyekiti wetu wa Mkoa, wameshindwa kujua jimbo la Bunda
msemaji wa chama au mkoa ni nani, wao badala ya kufuata katiba, wameshindwa
kujua katiba inasemaje kuhusu malalamiko yoyote.
“Wao
hawakuona katiba inasemaje na kanuni za chama zinasemaje na taratibu
zinasemaje, kuhusu malalamiko yoyote kama yalikuwepo ili waweze kuyafanyia
kazi, badala yake kilichofanyika ni udhalilishaji.
“Mimi
ni mwachama mwaminifu wa Chadema, nimekitumikia chama kwa kipindi cha miaka
zaidi ya kumi, lakini leo Bunda imekuwa shamba la bibi, maamuzi ya mtu ndiyo
yanayokuja kulitengeneza jimbo la Bunda, Kamati Tendaji ya jimbo la Bunda
ilifanya uteuzi wake wa awali kupitia kura za maoni.
“Walimaliza
kura za maoni wakaenda kwenye kamati tendaji, mimi kama Katibu wa Wilaya
naletewa mapendekezo ya kamati tendaji ndiyo ninayafanyia maamuzi, nilichukua
majina ya wagombea nikayapeleka kwenye tume kwenda kuyatambulisha, lakini
kilichotokea Mkoa na Kanda na Naibu Katibu Mkuu wakatoa maelekezo mengine
mbadala, akaletwa mtu ndani ya ofisi yangu bila kunishirikisha wala hata kupewa
barua ya kunitambulisha.
“Lakini
kilichofanyika huyo aliyeletwa akaanza kunielekeza, lakini mimi kama Katibu wa
Wilaya ninayejua utaratibu nilikataa. Kilichotokea nikiingia ofisini kwangu
pale naonekana kama mimi ni mgeni au mtu anayehitaji huduma pale, na
kilichotokea wakachonga muhuri mwingine wakatengeneza muhuri ndani ya muhuri
mwingine,” alidai.
Samwel
Alfred alisema;”Mimi ndiye Mwenyekiti wa Chadema Jimbo la Bunda, nimeamua
kujiuzulu kwa sababu kuna vitu vilivyonikera baada ya kuona kuna watu wanavunja
Katiba.
“Cha
kwanza tulipiga kura za maoni wakapatikana washindi watatu wakiwemo wawili
ambao wamekitumikia chama, lakini cha ajabu wakarudisha jina la mshindi wa tatu
(Esther Bulaya), hawakuvunja Katiba?
Cha
ajabu aliyerudishwa hakuonyesha ushirikiano na viongozi waliokuwepo, kwa
kuhofia kuwa walikuwa kambi nyingine kwamba watasababisha ashindwe,” alisema.
Aliongeza kuwa pia kwa upande wa wagombea udiwani, wagombea waliopendekezwa na
kamati tendaji pia majina yao yalibadilishwa na viongozi wa mkoa, kanda na hata
taifa.
“Mimi
kama kiongozi niliyepigania chama hiki niliyepata kesi nyingi nimekaa magereza,
nimenyanyaswa nimepigwa na nimedhalishwa sana, leo hii nimeamua kujiuzulu,
lakini siyo kwamba naondoka peke yangu naondoka na makamanda wakiwemo wajumbe
wa Kamati ya Utendaji na Katibu wa Vijana (Bavicha), kwa hiyo robo tatu ya
kamati tendaji yote tumejiuzulu.
Katibu
Mwenezi wa Jimbo, Malibwa alisema; “’Sijaondoka peke yangu kama mnavyoona hapa
ndugu waandishi wa habari tunao viongozi wote wa kata 20 za jimbo la Bunda,
wakiwemo wenyeviti wa kata, makatibu wa kata, kwa ujumla kamati ya utendaji
yenye watu 17, mimi mwenezi, mwenyekiti wangu na wajumbe wengine tumeondoka
wamebaki watu watatu tu,” alisema.( startvtz)
0 comments:
Post a Comment